|
Jeshi la polisi mkoani Geita, limefanikiwa kulitia mbaroni jambazi moja
na kufanikisha kuzinasa bunduki sita ambazo ziliporwa na kundi la
majambazi usiku wa kumkia juzi katika kituo cha polisi wilayani Bukombe.
Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, alisema
jambazi hilo lilinaswa porini likiwa na silaha hizo ambazo ziliporwa
baada ya kuvamia kituo hicho na kuua polisi wawili papo hapo na kujeruhi
wengine wawili.
“Hawa majambazi wameonekana kujichanganya na wafugaji waliopo mipakani,
hivyo uhalifu wao wakifanya wanakimbilia kwa wafugaji…natangaza kuanzia
sasa wale wafugaji waliopo pembezoni mwa mipaka kuondoka mara moja ili
kutowapa nafasi majambazi kujificha,” alisema Mangu.
Hata hivyo, Mangu alisema baadhi ya mapori ya akiba katika mikoa ya
Kagera, Geita, Kigoma na Shinyanga yamegeuzwa maficho ya wahalifu na
mikakati inafanyika kutafuta ufumbuzi wa kudumu badala ya ukanda wa
mapori hayo kutangazwa kanda maalum ya mikoa ya kipolisi.
|
Akikwepa kulihusisha tukio la juzi la kuvamiwa kwa kituo cha polisi na
kuuawa kwa polisi wawili na kujeruhi wengine na kuondoka silaha
mbalimbali zikiwamo bunduki aina ya SMG, risasi na mabomu ya kutupa kwa
mkono, alisema matokeo ya uchunguzi ndiyo yatabainisha ukweli halisi.
Alisema baadhi ya wahalifu hutoka nchi jirani na kushirikiana na baadhi
ya wenyeji kwa kutumia mapori ya akiba na baadhi ya hifadhi kujificha
kabla na baada ya kutekeleza uhalifu wao.
Alisema operesheni rasmi ya kuwasaka watuhumiwa waliohusika na tukio la
uvamizi wa kituo cha polisi cha Bushirombo imeanza baada ya kikao cha
kamati ya ulinzi na usalama cha mkoa wa Geita kufanyika juzi.
Juzi watu wanaoaminika ni majambazi walivamia kituo cha polisi cha
Bushirombo ambacho makao makuu ya polisi wilaya ya Bukombe kushambulia
na kuwaua polisi WP 7106 Uria Mwandiga na G.2615 Pc Dustani Kimati.
No comments:
Post a Comment